Storm FM

Nyang’hwale yatoa kipaumbele kwa elimu maalum

7 June 2026, 2:00 pm

Wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Wadau wamefanikiwa kuchangia milioni 37 zitakazotumika kuboresha miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa uzio katika bweni la wasichana

Na Mrisho Sadick:

Serikali Mkoani Geita imewahimiza wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kuhakikisha wanawapeleka shule ili wapate haki yao ya msingi ya elimu kwakuwa serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia nakufundishia kwa watoto wenye mahitaji maalumu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ametoa wito huo Juni 05,2026 katika shule ya msingi Bupamba kitengo Cha Elimu maalumu alipotembelea kukagua maendeleo ya wanafunzi hao kabla ya hafla ya chakula Cha Mchana iliyoandaliwa na wadau wa Elimu pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale iliyokuwa na lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watoto hao huku Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Emmanuel Erasto ameiomba serikali kuhakikisha miundombinu ya shule hiyo inaboreshwa.

Viongozi na wadau wa elimu wilayani Nyang’hwale wakiwa katika ziara ya mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Husna Toni amesema kwa kushirikiana na wadau wa elimu, wakiwemo wachimbaji wadogo, wamefanikiwa kuchangia milioni 37 zitakazotumika kuboresha miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa uzio katika bweni la wasichana, ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na kugharamia bima za afya za NHIF kwa wanafunzi hao. 

Wanafunzi wa shule ya msingi Bupamba wakiwa katika hafla ya mkuu wa mkoa na wanafunzi wenye mahitaji maalum. Picha na Mrisho Sadick

Baadhi ya wadau waliofanikisha zoezi hilo akiwemo Misana Nyabange  Katibu wa chama cha Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Mkoa wa Geita   na Salima Mipawa Mdau wa elimu wamesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanapata elimu katika mazingira bora, salama na rafiki.

Ripoti kamili na Mrisho Sadick