Storm FM

DED Manispaa ya Geita ahimiza nidhamu na maadili kwa walimu

17 April 2026, 2:03 pm

Mkurugenzi wa manispaa ya Geita Yefred Myenzi akihutubia katika maadhimisho ya siku ya mwalimu. Picha na Ester Mabula.

“Ni muhimu kujiweka katika mazingira yenye kuheshimika kwenye Jamii kwa kuzingatia nidhamu ambayo hiyo itasaidia hata kwenye kuongeza ufaulu wa wanafunzi” – DED Myenzi

Na: Ester Mabula

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya manispaa ya Geita Ndg. Yefred Myenzi amewataka walimu kuzingatia nidhamu na maadili ya kazi akieleza kuwa ndiyo silaha kuu ambayo itasaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi sambamba na kuweka hadhi ya mwalimu kwenye Jamii.

Ndg. Myenzi ameyasema hayo April 16, wakati akihutubia siku ya mwalimu iliyoandaliwa na idara ya elimu sekondari, halmashauri ya manispaa ya Geita iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana Nyankumbu.

Sauti ya DED Yefred Myenzi
Mchezo wa mpita wa pete ukiendelea uliochezwa na walimu wanawake. Picha na Ester Mabula

Maadhimisho ya siku hiyo yaliambatana na bonanza la michezo mbalimbali sambamba na utoaji wa zawadi mbalimbali kwa walimu na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, ambapo mwalimu wa somo la Kiswahili kutoka shule ya Ihanamilo Mwita Magige amekabidhiwa zawadi ya pikipiki kutokana na jitihada za kuongeza ufaulu katika somo lake.

Sauti ya Mwalimu Mwita Magige
Mwalimu Mwita Magige akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kukabidhiwa zawadi. Picha na Ester Mabula

Baadhi ya walimu, mkuu wa shule ya wasichana ya Nyankumbu Khadija Kayanda na mwalimu Festo Nteze kutoka shule ya Ihanamilo wamepongeza uwepo wa siku hiyo wakieleza itatoa motisha kwa walimu kufanya vizuri zaidi.

Sauti ya walimu
Zawadi mbalimbali zikiendelea kutolewa kwa walimu waliofanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani. Picha na Ester Mabula