Storm FM

RPC Geita asema Polisi kuingia bure kutoka bure

19 June 2026, 2:06 pm

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita akizungumza na wakazi wa Bunigonzi wilayani Mbogwe. Picha na Mrisho Sadick

Jeshi la polisi Geita latoa tamko kutokana na madai ya baadhi ya wananchi kulalamika kuwa ukihitaji huduma za kipolisi kama usipokuwa na pesa utapata changamoto sana kushughulikiwa tatizo lako.

Na Mrisho Sadick:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo ameendelea kusisitiza kuwa huduma zote za kipolisi zinatolewa bure ikiwemo huduma ya dhamana.

Kamanda Jongo ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Bunigonzi Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela.

Viongozi na wananchi wa Bunigonzi wakiwa kwenye ziara ya Mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Amesema kuwa hakuna mwananchi anayepaswa kutozwa fedha kwa ajili ya kupata dhamana au huduma nyingine yoyote ya kipolisi , amewataka wananchi kutoa taarifa kwake mara moja endapo watatakiwa kutoa fedha ili kupata dhamana au huduma yoyote kutoka kwa Jeshi la Polisi.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Geita
Viongozi na wananchi wa Bunigonzi wakiwa kwenye ziara ya Mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Katika hatua nyingine Kamanda Jongo amewataka wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao wa malezi kwa watoto nakwamba  Jeshi la Polisi limeanzisha oparesheni maalum ya kuwasaka na kuwakamata watoto wanaozurura mitaani nyakati za usiku, pamoja na kuwabaini wazazi au walezi wao ili wachukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.