Storm FM
Storm FM
22 June 2026, 5:41 pm

Serikali mkoani Geita imevalia njuga suala la kuboresha miundombinu baada ya Geita Gold kupanda ligi kuu soka ya NBC Tanzania bara.
Na: Ester Mabula
Halmashauri ya Manispaa ya Geita Mkoani Geita imepanga kutumia zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya maboresho ya uwanja wa Nyankumbu Girls utakao tumika kwa michezo ya ligi kuu msimu ujao baada ya timu hiyo kurejea ligi kuu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amebainisha hayo wakati wa hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa kwa ajili ya kuipongeza Geita Gold FC baada ya kutwaa ubingwa wa Championship na kufuzu kurejea Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Geita Yefred Myenzi amesema baraza la madiwani la manispaa ya Geita limeridhia gharama za awali za maboresho ikiwa ni sehemu ya ushauri wa Rais wa TFF Wallace Karia kutaka uwanja huo ufanyiwe maboresho kadhaa kabla ya ligi kuu msimu ujao kuanza.
Katika hatua Nyingine Mkuu wa Mkoa wa Geita amesema wakati uwanja wa Nyankumbu ukifanyiwa maboresho mkandarasi wa ujenzi wa Uwanja wa Magogo unaotarajiwa kutumiwa na timu hiyo atakabidhiwa eneo la mradi Julai 6, 2026 ili kuanza kazi ya ujenzi inayotarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi sita.
Kwa upande wake Kocha mkuu wa Geita Gold FC Zubeir Katwira amesema mafanikio ya timu hiyo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa klabu, Halmashauri ya Manispaa ya Geita, wadhamini na mashabiki waliokuwa bega kwa bega katika kipindi chote cha msimu.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Mkoa wa Geita Titus Kabuo amewatoa wasiwasi wapenzi na mashabiki wa Geita Gold FC kuwa chama hicho kitakuwa bega kwa bega na timu hiyo kuliko wakati wakati mwingine wowote uliopita kuhakikisha inafanya vizuiri.