Storm FM

CCM Geita yalaani tukio la binti kubakwa kisha mtuhumiwa kuomba malipo

3 June 2026, 1:38 pm

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nocholaus Kasendamila akizungumza katika mkutano uliohusisha viongozi mbalimbali wilayani Chato. Picha na Mrisho Sadick

Na: Mrisho Sadick

Mwanafunzi wa shule ya sekondari katika kijiji cha Imalabupina wilayani Chato mkoani Geita anadaiwa kufanyiwa ukatili wa kubakwa ambapo bada ya tukio hilo mtuhumiwa alidai kiasi cha shilingi 300,000 ili asimdhuru.

Inadaiwa kuwa tukio hilo limetokea Mei 31, 2026 ambapo mwanafunzi huyo alikuwa akirejea nyumbani kuchukua madaftari aliyosahau shuleni ndipo alipokutana na mtu huyo, ambaye tayari amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi.

Katika tukio hilo, binti huyo alijeruhiwa mkononi kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali alipokuwa akijaribu kujinasua.

Binti aliyefanyiwa ukatili wa kutekwa na kubakwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). Picha na Mrisho Sadick

Kufuatia tukio hilo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Geita kimekemea ukatili huo, kikilaani tukio la mwanafunzi huyo kutekwa na kufanyiwa ukatili huo ambapo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila, ametembelea familia ya mtoto huyo na kutoa pole, akisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kushirikiana katika kutoa ushahidi mahakamani ili kuhakikisha haki inatendeka.

Sauti ya Ripoti kamili na Mrisho Sadick