Storm FM

RC Shigela apiga marufuku wajawazito kutozwa pesa Bukombe

15 June 2026, 12:12 am

Wakazi wa Kijiji cha Msangila wilayani Bukombe wakiwa katika mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Sera ya afya nchini wanawake wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na wazee wanapaswa kupata huduma za matibabu bure

Na Mrisho Sadick:

Wakazi wa vijiji vya Bugelenga na Msangila wilayani Bukombe mkoani Geita wamelalamikia kutozwa fedha wanapohitaji huduma za kliniki kwa wanawake wajawazito na watoto  pamoja na kutoridhishwa na lugha zisizofaa zinazodaiwa kutumiwa na baadhi ya wauguzi wakati wa utoaji wa huduma za Afya.

Wananchi hao wametoa malalamiko hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela wilayani Bukombe. Wamesema wamekuwa wakitozwa kiasi cha fedha kinachofikia shilingi 40,000, kutegemeana na umri wa ujauzito.

Akizungumza katika ziara hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dk. Omari Sukari amesema kuwa kwa mujibu wa sera ya afya nchini wanawake wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na wazee wanapaswa kupata huduma za matibabu bila malipo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dk. Omari Sukari akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi Bukombe. Picha na Mrisho Sadick

Kutokana na malalamiko hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha anafuatilia na kutatua changamoto hiyo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ili wananchi wapate huduma kwa mujibu wa sera na taratibu zilizowekwa.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bulega Bukombe. Picha na Mrisho Sadick

Katika hatua nyingine Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo amewataka wazazi na walezi wilayani Bukombe kuimarisha malezi ya watoto wao nakwamba Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni maalumu ya kuwasaka watoto wanaoishi mitaani pamoja na kuwabaini wazazi au walezi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao wa malezi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskas Muragili amesema serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa soko la kisasa, kituo cha mabasi, ofisi ya Mkuu wa Wilaya na jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.

Ripoti kamili ya stori hii na Mrisho Sadick