Storm FM

CRDB yajenga madarasa ya milioni 50 shule kongwe ya Fulwe Geita

27 April 2026, 9:37 pm

Mbunge Musukuma akikata utepe wakati akikabidhi madarasa mawaili yaliyojengwa na Benki ya CRDB Nzera. Picha na Mrisho Sadick

Shule ya Msingi Fulwe iliyoanzishwa mwaka 1,956 imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya majengo hali iliyokuwa ikiathiri mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi

Na Mrisho Sadick – Geita

Benki ya CRDB imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii baada ya kukabidhi madarasa mawili yenye thamani ya shilingi milioni 50 pamoja na madawati 30 katika Shule ya Msingi Fulwe iliyopo Kata ya Nzera Wilaya ya Geita.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Joseph Musukuma amepongeza hatua ya CRDB akisema uwekezaji huo ni mfano bora kwa taasisi nyingine kushiriki kikamilifu katika kuboresha huduma za kijamii hususani elimu.

Sauti ya Mbunge Musukuma
Mbunge Musukuma , maafisa wa CRDB na viongozi mbalimbali wakiwa katika uzinduzi wa madarasa mawaili yaliyojengwa na Benki ya CRDB Nzera. Picha na Mrisho Sadick

Sambamba na hayo Mbunge Musukuma ameahidi kuchangia shililingi milioni 30 yeye pamoja na familia yake kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa madara mengine mawili , amesema ubora na thamani ya majengo yaliyotekelezwa na CRDB unapaswa kuigwa na watendaji wa serikali katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa gharama nafuu na zenye ufanisi.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa CRDB ambae ni Mkurugenzi wa TEHAMA Edward Mpina amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uwekezaji kwa jamii ya benki hiyo, ambapo hutenga takribani asilimia 1 ya faida baada ya kodi kila mwaka kusaidia sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu nakwamba itaendelea kufanya hivyo.

Sauti ya Mkurugenzi wa TEHAMA CRDB
Wanafunzi wa shule ya msingi Fulwe wakiwa katika hafla ya kukabidhiwa madarasa mawili yaliyojengwa na Benki ya CRDB. Picha na Mrisho Sadick

Aidha meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi Jumanne Wagana ameongeza kuwa benki hiyo itaendelea kuona umuhimu wa kuwekeza katika elimu kama msingi wa maendeleo endelevu ya taifa nakwamba mradi huo utakuwa chachu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika shule hiyo.

Sauti ya Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi
Muonekano wa madara mawili yaliyojengwa na Benki ya CRDB Katika shule ya msingi Fulwe Kata ya Nzera. Picha na Mrisho Sadick

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Leonard Amos na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo Said Said na Jeviva Salala wameipongeza CRDB kwa msaada huo wakisema umeleta matumaini mapya ya kujifunza katika mazingira bora zaidi kwakuwa baadhi ya madarasa katika eneo hilo yamejengwa na wakoloni.