Storm FM
Storm FM
7 June 2026, 3:33 pm

Usiku wa June 06, 2026 zimetolewa tuzo za malkia wa dhahabu kwa kuthamini jitihada za wanawake katika sekta mbalimbali mkoani Geita.
Na: Ester Mabula
Mkurugenzi na mmiliki wa Kadama English Medium Primary School Bi. Leticia Pastory ametunukiwa tuzo ya Mmiliki bora wa shule wa kike mkoa wa Geita 2026 (CEO Bora) ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuendeleza sekta ya elimu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa Juni 6, 2026 na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa na Mbunge Mary Chatanda katika Tamasha la Malkia wa Dhahabu (Geita Women Festival 2026) lililofanyika katika Ukumbi wa Golden Social Hall manispaa ya Geita.
Tuzo hizo zimeandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Geita Women and Youth Foundation chini ya Mkurugenzi wake Cecylia Miraji, kwa lengo la kutambua wanawake wenye mchango mkubwa na chanya katika jamii kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na jamii akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela, Mbunge wa Geita Mjini Chacha Wambura pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Yefred Myenzi.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Leticia alisema heshima hiyo ni matokeo ya juhudi za muda mrefu za kuinua kiwango cha elimu katika Mkoa wa Geita kupitia Kadama English Medium Primary School.

Alisema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma na kujijengea sifa ndani na nje ya mkoa kutokana na ubora wa ufundishaji na mazingira bora ya kujifunzia.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya shule hiyo ni mwaka 2018 ilipotoa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa na mwingine aliyeshika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya elimu ya msingi hatua iliyochangia kuitangaza shule hiyo kwenye ramani ya elimu nchini.
Leticia amesema tuzo hiyo itakuwa chachu ya kuendelea kuimarisha ubora wa elimu na kuwahamasisha wanawake wengine kutumia nafasi walizonazo kuleta maendeleo katika jamii.
