Storm FM

Kituo cha mafuta chateketea kwa moto Geita

10 July 2026, 7:10 pm

Muonekano wa Kituo cha mafuta Lake Energies kilivyo teketea kwa moto. Picha na Kale Chongela

Chanzo cha moto huo kilitokana na gari aina ya Center lenye namba za usajili T799 BEB, ambalo lilikuwa limeingia katika kituo hicho kujaza mafuta.

Na Kale Chongela:

Kituo cha mafuta cha kampuni ya Lake Energies, kilichokuwa kikifahamika awali kama Lake Oil, kilichopo Mtaa wa Bombambili, Halmashauri ya Manispaa ya Geita kimeteketea kwa moto.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 10, 2026 Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Mrakibu Msaidizi Kenneth Mwakasitu, amesema kikosi cha Zimamoto kilifika kwa haraka eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti moto huo.

Amesema chanzo cha moto huo kilitokana na gari aina ya Center lenye namba za usajili T799 BEB, ambalo lilikuwa limeingia katika kituo hicho kujaza mafuta, wakati zoezi la kujaza mafuta likiendelea gari hilo lilipata hitilafu na kuwaka moto, hali iliyosababisha moto kusambaa na kuteketeza sehemu kubwa ya kituo hicho.

Sauti ya Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita

Jeshi la Zimamoto likiendelea na zoezi la kuzima moto katika kituo cha mafuta Lake Energies. Picha na Kale Chongela

Kwa upande wake, kiongozi wa kituo cha Lake Energies amesema taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha moto kilihusishwa na hitilafu katika betri la gari hilo wakati likiwa linaendelea kujazwa mafuta, ingawa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo halisi.

Sauti ya kiongozi wa kituo cha Lake Energies

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema moto ulizuka ghafla na kusababisha taharuki miongoni mwa wananchi pamoja na watumiaji wa barabara waliokuwa karibu na eneo hilo.

Sauti ya mashuhuda wa tukio