Storm FM
Storm FM
8 June 2026, 11:15 am

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku likiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kutoa taarifa zitakazosaidia kukamilisha uchunguzi na kuhakikisha haki inatendeka.
Na Mrisho Sadick:
Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa ambae ni Diwani wa Kata ya Kalangalala Manispaa ya Geita Reuben Sagayika amelaani vikali tukio la kubakwa kwa mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Ichwankima wilayani Chato, huku akiiomba Halmashauri ya Wilaya ya Chato kuharakisha ujenzi wa shule ya sekondari katika kijiji hicho ili kupunguza changamoto za umbali na kuwalinda wanafunzi wa kike dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumzia tukio hilo katika kijiji hicho Sagayika amesema ni muhimu mamlaka husika kuchukua hatua madhubuti za kulinda usalama wa wanafunzi, huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa shule karibu na makazi ya wananchi utasaidia kupunguza hatari zinazowakabili wanafunzi wanapolazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni.

Mwanafunzi huyo alikutana na mtuhumiwa njiani ambaye alimkamata na kumvutia vichakani ndani ya eneo la hifadhi ya taifa ya Burigi Chato kabla ya kutekeleza kitendo hicho cha kikatili hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia na linaendelea kumhoji Peter Willium (28) mkazi wa Itale wilayani Chato kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi huyo.