Storm FM

Jumuiya ya wazazi yawaonya wanaotumikisha watoto migodini Geita

11 August 2026, 7:05 pm

Wajumbe wa kikao cha baraza la jumuiya ya wazazi mkoa wa Geita wakiwa kwenye kikao. Picha na Mrisho Sadick

Kikao hicho kimeweka mkakati wa kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata haki yao ya msingi ya elimu mkoa wa Geita

Na Mrisho Sadick:

Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita imewaonya baadhi ya wazazi na walezi wanaoendelea kuwatumikisha watoto katika shughuli za migodini, uchungaji wa mifugo, uvuvi pamoja na biashara katika vituo vya mabasi.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Geita, Lucas Mazinzi, baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Jumuiya hiyo kilichofanyika katika Ofisi mpya ya CCM Mkoa wa Geita.

Mazinzi amesema wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu, badala ya kuwashirikisha katika shughuli za kiuchumi zinazoweza kuhatarisha maisha yao na kuathiri mustakabali wao.

Wajumbe wa kikao cha baraza la jumuiya ya wazazi mkoa wa Geita wakiwa kwenye kikao. Picha na Mrisho Sadick

Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wamesema juhudi mbalimbali zinazofanywa zimeanza kupunguza ajira za watoto, huku wakisisitiza kuwa hawatakubali kuona watoto wenye umri wa kwenda shule wakinyimwa haki yao ya kupata elimu.

Wamesema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukabiliana na ajira za watoto na kuhakikisha mazingira bora yanapatikana kwa watoto ili waweze kusoma na kukua katika mazingira salama.

Wajumbe wa kikao cha baraza la jumuiya ya wazazi mkoa wa Geita wakiwa kwenye kikao. Picha na Mrisho Sadick

Mbali na mapambano dhidi ya ajira za watoto, Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Geita imeeleza kuwa inaendelea kujidhatiti katika ujenzi wa nyumba za watumishi pamoja na kuwekeza katika vitega uchumi mbalimbali kwa lengo la kuongeza uwezo wa kifedha na kupunguza utegemezi.

Ripoti ya Stori hii na Edga Rwenduru