Storm FM
Storm FM
10 September 2026, 4:40 pm

Uongozi wa mtaa pia umesisitiza ushirikiano wa wananchi katika kusafisha mitaro na kuondoa taka zinazoweza kuziba njia za maji, huku wakazi wakitakiwa kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi kabla na wakati wa msimu wa mvua.
Na Mrisho Sadick:
Mtaa wa Mbugani katika Manispaa ya Geita Mkoani Geita ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na mafuriko kila msimu wa mvua, hali inayoweka wakazi wake katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko pamoja na madhara mengine yanayotokana na mafuriko.
Mtaa huo una wakazi zaidi ya 7,000 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, huku Serikali ikitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa za El Niño, wananchi wa eneo hilo wameanza kuchukua hatua mbalimbali za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.
Mwandishi wetu Lydia Mgusi ametembelea mtaa huo na kuzungumza na baadhi ya wakazi ili kufahamu namna wanavyojiandaa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kusababishwa au kuchochewa na mafuriko, uchafuzi wa mazingira na matumizi ya maji yasiyo salama.
Baadhi ya wakazi akiwemo Jonathan Mujwauzi wameeleza kuwa wanafahamu magonjwa ya mlipuko pamoja na sababu zinazoweza kusababisha kuenea kwa magonjwa hayo hasa katika kipindi cha mvua kubwa na mafuriko.
Wakazi hao wameeleza umuhimu wa kuzingatia usafi wa mazingira, kutumia maji salama, kutunza vyakula kwa usahihi na kuhakikisha mazingira ya makazi yanakuwa safi ili kupunguza uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa.
Kwa upande wake Leonida Machumu ambaye ni Mama Lishe katika eneo hilo amesema amekuwa akichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha anakinga afya yake pamoja na afya za wateja wanaofika kupata huduma ya chakula katika eneo lake.
Machumu ameeleza kuwa anazingatia usafi wa vyombo vya chakula, usafi wa eneo la biashara, utunzaji wa chakula na kuhakikisha chakula kinakuwa katika mazingira salama ili kuzuia uchafuzi ambao unaweza kusababisha magonjwa kwa walaji.
Akizungumzia hali ya Mtaa wa Mbugani Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Jumanne Bayasabe amesema eneo hilo liko katika bonde na limekuwa likikumbwa na mafuriko mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua.
Amesema uongozi wa mtaa umeendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika usafi wa mazingira na kuchukua hatua za mapema ili kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuwaagiza wananchi kufungua na kusafisha mitaro, kuondoa taka zinazoziba njia za maji na kuhakikisha njia zote zinazotumika kupitisha maji zinaendelea kuwa wazi.
Hatua hizo zinalenga kupunguza uwezekano wa maji kutuama na kujaa katika maeneo ya makazi, hali ambayo inaweza kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko.
Kwa hali hiyo maandalizi ya mapema yanaonekana kuwa njia muhimu ya kupunguza athari za mafuriko na magonjwa ya mlipuko katika Mtaa wa Mbugani hasa ikizingatiwa kuwa eneo hilo limekuwa likikumbwa na mafuriko mara kwa mara kila msimu wa mvua.