Storm FM
Storm FM
23 September 2026, 2:26 pm

Kupitia Program hiyo wanafunzi mbalimbali waliokuwa wamekata tamaa na kukatisha masomo sasa wamerudi shule na wanaendelea kufanya vizuri.
Na Mrisho Sadick:
Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha kundi la Vyuo na Vyuo Vikuu nchini Tanzania Mhe. Selina Kingalame amewataka wanafunzi wa shule za sekondari wilayani Nyang’hwale mkoani Geita kutumia fursa ya ukuaji wa teknolojia na mitandao ya kijamii kuongeza ujuzi na kuboresha ufanisi wa kujifunza badala ya kuitumia kwa mambo yasiyofaa.
Kingalame ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa Programu ya “Genz Soma kwa Malengo”uliofanyika katika Shule ya Sekondari Kanegele wilayani Nyang’hwale ambapo amesema matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kuwasaidia wanafunzi kupata maarifa na taarifa mbalimbali zinazoweza kuongeza uelewa wao katika masomo na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha ya baadaye.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Husna Toni amesema matarajio ya Halmashauri hiyo ni kuona wanafunzi wakisoma kwa malengo na kuzingatia elimu kama msingi muhimu wa maisha yao ya baadaye.
Awali Mratibu wa Programu hiyo Imelda Frank amesema “Genz Soma kwa Malengo” ni maono ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Bi Husna Toni ya kubadili mtazamo wa jamii kuhusu mfumo mzima wa elimu nakuongeza ufaulu kwenye shule za sekondari na msingi nakwamba ilianzishwa Januari 2026 inatekelezwa na watalaamu na idara kutoka vitengo mbalimbali Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale.
Amesema utekelezaji umeanza katika shule saba za sekondari za Kanegele , Busolwa ,Mwingilo , Shabaka,Bukwimba, Msalala na Nyang’hwale kwa malengo mahususi ya kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi , kuwapatia hamasa na elimu ya kupenda shule , kuwajengea uwezo juu ya fursa za elimu zinazopatikana kwa wanafunzi wanaofany vizuri , kubaini nakutatua changamoto ambazo ni kikwazo kwa wanafunzi, kuwajengea uwezo wa kujitegemea kwa kuwapatia ujuzi wa kutengeneza sabuni za maji , unga wa lishe , ufugaji wa nyuki na kilimo cha bustani.

Wanafunzi wa shule za sekondari wilayani humo wameipongeza serikali kwa kuanzisha program hiyo kwani imekuwa msaada kwa wanafunzi ambao walikuwa wamekata tamaa na wale waliokuwa wamekatisha masomo kutokana na ugumu wa maisha kwenye familia zao.