Storm FM
Storm FM
6 November 2026, 2:31 pm

Mradi huo utaongeza uzalishaji wa maji hadi kufikia lita milioni 45 kwa siku na utahudimia kata zote 13 za Manispaa ya Geita pamoja na vijiji 19 vya Halmashauri ya Wilaya ya Geita
Na Mrisho Sadick:
Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria wilaya ya Geita Mkoani Geita wameiomba Serikali kuhakikisha wanapewa kipaumbele cha kusambaziwa maji pindi mradi wa maji wa miji 28 utakapokamilika ili kuwaondolea changamoto ya kushambuliwa na wanyama wakali wakiwemo mamba na viboko wanapokwenda kuchota maji ziwani.
Wakazi hao wametoa ombi hilo wakati wa ziara ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa CCM Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ndugu Rajab Abdallah alipotembelea na kukagua mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 124 ambao umefikia zaidi ya asilimia 80 ya utekelezaji.

Mwakilishi wa mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Geita GEUWASA amesema mahitaji ya maji kwa mji wa Geita lita milioni 23 kwa siku huku uzalishaji ukiwa ni lita milioni 8 tu nakwamba mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji zaidi ya lita milioni 45 kwa siku nakwamba mradi huo utahudumia zaidi ya watu laki saba.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Ndugu Rajab Abdallah amesema dhamira ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha changamoto ya maji iliyowasumbua wananchi kwa muda mrefu wanaoishi pembezoni ya vyanzo vya maji vya uhakika kama Ziwa inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
