Storm FM

RC Mnyeti arejesha nyumba ya Fatuma aliyopokonywa Kanyara

28 September 2026, 1:18 pm

Bi Fatuma Seif akiwa katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa mkoa katika Kata ya Kanyara wilayani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Fatuma atembea wilaya zote kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Geita kwenye mikutano yake ili kutafuta haki yake baada ya kufukuzwa kwenye nyumba yake.

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexander Mnyeti amefanikiwa kurejesha nyumba ya Bi Fatuma Seif mkazi wa Kata ya Kanyara Manispaa ya Geita aliyokuwa amenyang’anywa ili kufidia deni la mkopo wa shilingi milioni 18 uliokopwa na mumewe bila kumshirikisha.

Fatuma amesema mwaka 2023 mumewe alikopa kiasi hicho cha fedha lakini baadaye alishindwa kurejesha mkopo huo kwa wakati hali ambayo ilisababisha nyumba yao kuwa katika hatari ya kuchukuliwa kwa ajili ya kufidia deni hilo.

Kwa mujibu wa Fatuma baada ya mumewe kushindwa kurejesha mkopo huo licha ya kuwa na kaya mbili  aliondoka na kumuacha yeye akiwa katika hali ngumu huku akihangaika kutafuta haki yake kupitia vyombo mbalimbali bila kupata suluhisho la kudumu.

Mkuu wa mkoa wa Geita Alexander Mnyeti akiwa katika mkutano wa hadhara Kata ya Kanyara. Picha na Mrisho Sadick

Baada ya suala hilo kufikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexandra Mnyeti aliingilia kati na kusaidia kuzuia nyumba hiyo kunyang’anywa hatua iliyompa Fatuma nafuu na kumwezesha kuendelea na maisha katika makazi yake.

Mnyeti amewataka watendaji wa kata na vijiji kuwa karibu na wananchi na kushughulikia changamoto zinazoweza kutatuliwa katika ngazi zao, badala ya kusubiri kila tatizo lifikishwe kwa viongozi wa ngazi za juu.

Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick