Storm FM
Storm FM
26 October 2026, 12:49 pm

Hata hivyo bado haijafahamika ndege huyo alikuwa wa aina gani na ni nini kilichosababisha tabia hiyo ya kuwashambulia wananchi.
Na Mrisho Sadick:
Ndege wa ajabu aliyekuwa akiwashambulia wananchi kwa kuwapiga kichwani katika mtaa wa Geita Road kata ya Nyatukala wilayani Sengerema mkoani Mwanza ameuawa kwa kupigwa mawe na wananchi wa eneo hilo.
Wakizungumza kuhusu tukio hilo baadhi ya wananchi wamesema kuwa hali ya amani imerejea katika mtaa huo na shughuli za kila siku zinaendelea kama kawaida baada ya kuondolewa kwa hofu iliyokuwa imetanda kutokana na mashambulizi ya ndege huyo.
Kabla ya kuuawa kwake ndege huyo alisababisha taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, baadhi ya wananchi waliodai kushambuliwa na ndege huyo wamesimulia namna walivyokuwa wakikumbana na mashambulizi hayo yaliyowatia hofu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Geita Road Pelana Bagume amethibitisha kuuawa kwa ndege huyo baada ya wananchi kumshambulia kwa mawe.