Storm FM

Wasiohudhuria misiba kukiona cha moto Geita Road

2 November 2026, 4:13 pm

Picha hii imetengenezwa kupitia mtandao kwahyo siyo halisi

Wananchi wameiomba Serikali kuongeza usimamizi wa sheria ndogo za kijamii na kuhakikisha zinatekelezwa ipasavyo ikiwemo kuweka faini

Na Mrisho Sadick:

Uongozi wa Mtaa wa Geita Road Kata ya Nyatukala Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza umetangaza kuchukua hatua kali dhidi ya wananchi wenye tabia ya kutohudhuria misiba inayotokea katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa mtaa huo Pelana Bagume ambaye amesema hatua hiyo inalenga kukomesha tabia ya baadhi ya wananchi kushindwa kujitokeza kushiriki katika misiba ya wenzao licha ya umuhimu wa mshikamano na kusaidiana katika nyakati za majonzi.

Bagume amewataka wananchi kuachana na tabia hiyo na kuzingatia wajibu wao wa kijamii akionya kuwa hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuongeza usimamizi wa sheria ndogo za kijamii na kuhakikisha zinatekelezwa ipasavyo ikiwemo kuweka faini kwa wananchi watakaobainika kutoshiriki katika misiba, ili kuimarisha mshikamano na ushirikiano katika jamii.

Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick