Storm FM

Dkt. Mwigulu ahitimisha maonesho Geita, GGML ikijivunia udhamini mkuu

4 October 2026, 1:09 am

Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akihutubia wananchi (hawapo pichani). Picha na Ester Mabula

Maonesho ya 9 ya teknolojia ya madini yamehitimishwa mkoani Geita ambapo kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ikiendelea kujivunia kuwa mdhamini mkuu wa maonesho hayo.

Na: Ester Mabula

Maonesho hayo yamehitimishwa Oktoba 03, 2026 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.  Mwigulu Lameck Nchemba kwa niaba ya Rai Samia Suluhu ambapo yalihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, teknolojia na ubunifu.

Ushiriki na udhamini wa GGML unaendelea kuonesha dhamira yake ya kushirikiana na wadau na serikali katika kuendeleza sekta ya madini nchini kuelekea dira ya Taifa ya maendeleo 2050 ambapo Mkurugenzi wa GGML Ashraf Suryaningrat ameeleza kuwa maonesho hayo yanawasaidia kueleza wananchi juu ya shughuli zao mbalimbali na kwamba kwao uchimbaji si tu kutoa dhahabu ardhini bali pia kuzingatia uchimbaji salama na kunufaisha Jamii inayozunguka mgodi huo.

Sauti ya mkurugenzi mtendaji wa GGML
Mkurugenzi mtendaji wa GGML Ashraf Suryaningrat akihutubia mbele ya wananchi na viongozi (hawapo pichani). Picha na Ester Mabula

Rais  wa Shirikisho la vyama vya wachimbaji wa madini nchini Tanzania (FEMATA) John Bina ameiomba serikali kupitia mabenki yote nchini kuweka mazingira ya kuweza kuwakopesha wachimbaji wadogo ili waweze kupata mitaji ya kufanya shughuli za uchimbaji huku waziri wa madini Anthony Mavunde akieleza kuwa tayari ameanza hatua za kufuta leseni zote ambazo haziendelezwi na wamiliki wake.

Sauti ya Rais wa FEMATA John Bina na waziri wa madini Anthony Mavunde
Waziri wa madini Anthony Mavunde akizungumza na wananchi na viongozi (hawapo pichani). Picha na Ester Mabula

Mgeni rasmi, Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba amesema serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kufanya mageuzi katika sekta ya madini ili kuongeza tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Sauti ya mgeni rasmi, waziri mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba