Storm FM

Bilioni 4.5 kujenga jengo la watoto njiti hospitali ya mkoa Geita

9 September 2026, 3:34 pm

Daktari bingwa wa watoto akitoa maelezo ya matumizi ya mashine za watoto waliozaliwa kabla ya muda. Picha na Mrisho Sadick

Kila mwezi hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita inapokea watoto waliozaliwa kabla ya muda kati ya 30 na 40 hali inayoashiria ongezeko la mahitaji ya huduma maalumu kwa watoto hao.

Na Mrisho Sadick:

Serikali imetenga Shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo maalumu litakalotumika kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye mahitaji maalumu katika Mkoa wa Geita ambapo ujenzi wa jengo hilo tayari umeanza na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2027.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omari Sukari amebainisha hayo baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kutoa msaada wa mashine mbili zinazotumika katika matibabu ya watoto waliozaliwa kabla ya muda pamoja na watoto wenye changamoto ya ugonjwa wa manjano.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU akikabidhi mashine za kuwasaidia watoto wachanga wenye mahitaji maalumu. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Watoto katika hospitali hiyo Dkt. Joyce Gimonge amesema wanapokea watoto waliozaliwa kabla ya muda kati ya 30 na 40 kila mwezi, hali inayoashiria ongezeko la mahitaji ya huduma maalumu kwa watoto hao.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Neema Mwakalyelye amesema taasisi hiyo imetoa mashine hizo mbili kupitia michango ya wafanyakazi wake, ikiwa ni sehemu ya misaada mbalimbali inayotolewa na TAKUKURU katika hospitali za mikoa nchini.

Mashine kwa ajili ya watoto waliozaliwa kabla ya muda iliyotolewa na TAKUKURU Mkoani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexander Mnyeti ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo na kuahidi kuwa serikali itanunua mashine nyingine nne ili kukamilisha idadi ya mashine 10 zinazohitajika hospitalini hapo.

Amesema baada ya mashine mbili kutolewa na TAKUKURU hospitali hiyo sasa ina jumla ya mashine sita, huku serikali ikilenga kuongeza mashine nyingine nne ili kukidhi mahitaji ya huduma kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda na wale wenye ugonjwa wa manjano.

Ripoti ya Stori na Mrisho Sadick