Storm FM

Waliotoa vibali vya ujenzi mikondo ya maji kikaangoni Geita

21 September 2026, 7:09 pm

Picha ya tukio la mvua mwaka 2024 katika mtaa wa Samina Manispaa ya Geita mkoani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Reuben Kwagwila amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Geita kuwatafuta na kuwakamata maafisa ardhi wa Manispaa ya Geita wanaodaiwa kushiriki kutoa vibali na hati miliki kwa watu waliojenga katika mikondo ya maji na maeneo ya mabonde.

Naibu Waziri Kwagwila ametoa agizo hilo baada ya kutembelea mitaa ya Mbugani, Moringe na Katundu katika Manispaa ya Geita ambayo imekuwa ikikumbwa na mafuriko mara kwa mara hususan wakati wa mvua kubwa.

Naibu Waziri akikagua mkondo wa maji katika Mtaa wa Mbugani Manispaa ya Geita. Picha na Mrisho Sadick

Aidha amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Yefred Myenzi kuanza mara moja utekelezaji wa mpango wa kuzibua, kusafisha na kurekebisha njia za maji kwa lengo la kupunguza athari za mafuriko katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba ameahidi kutekeleza maagizo hayo ikiwemo kuhakikisha maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko yanakuwa salama wakati na baada ya mvua kubwa za El Niño.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Reuben Kwagwila akizungumza baada ya ukaguzi. Picha na Mrisho Sadick

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbugani Jumane Bayasabe kwa niaba ya wenyeviti wa mitaa sita ameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto hiyo akieleza kuwa baadhi ya maeneo hayo ni hatarishi kwa usalama wa wananchi.

Awali wakazi wa Mtaa wa Mbugani walipata fursa ya kuwasilisha kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo mafuriko ya mara kwa mara pamoja na upungufu na changamoto za miundombinu ya maji.

Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick