Storm FM

DC Komba ataka wavuvi na wachimbaji waungwe WCF Geita

4 November 2026, 4:10 pm

Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya WCF. Picha na Mrisho Sadick

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa kuhusu mfumo wa fidia kwa wafanyakazi, namna mfuko unavyotoa fidia kwa waathirika wa ajali na magonjwa yatokanayo na kazi

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba ameutaka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuongeza juhudi za kuwafikia waajiri katika sekta zenye mazingira hatarishi ya kazi hususan sekta ya uvuvi na uchimbaji wa madini katika migodi midogo na ya kati ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata ulinzi na haki zao kwa mujibu wa sheria.

Komba ametoa rai hiyo leo Novemba 04,2026 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Rasilimali Watu na Maafisa Usalama na Afya Mahali pa Kazi kutoka sekta za umma na binafsi, yanayofanyika katika Manispaa ya Geita, mkoani Geita.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. Abdulsalaam Omar akiwa katika mafunzo. Picha na Mrisho Sadick

Amesema sekta hizo zina mazingira yenye vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kusababisha ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza elimu na uelewa kwa waajiri kuhusu wajibu wao katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. Abdulsalaam Omar ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa kuhusu mfumo wa fidia kwa wafanyakazi, namna mfuko unavyotoa fidia kwa waathirika wa ajali na magonjwa yatokanayo na kazi, pamoja na kuimarisha mbinu za kuzuia vihatarishi mahali pa kazi.

Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye mafunzo ya WCF Manispaa ya Geita Mkoani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka sekta za umma na binafsi wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema maarifa watakayoyapata watayatumia kuboresha mifumo ya usalama na afya katika maeneo yao ya kazi, pamoja na kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick