Storm FM
Storm FM
28 September 2026, 3:38 pm

Maonesho ya 9 ya madini yamezinduliwa rasmi Septemba 27, 2026 yakiwa na kaulimbiu isemayo “MADINI NI UTAJIRI, TUWAJIBIKE KWA PAMOJA TUFIKIE DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050” ambapo yanatarajiwa kuhitimshwa Oktoba 03, 2026
Na: Ester Mabula
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeendelea kushiriki katika maonesho ya madini ambayo hufanyika kila mwaka mkoani Geita yakikutanisha washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo Mkurugenzi mtendaji wa GGML Ashraf Suryaningrat amesema kuelekea dira ya taifa ya maendeleo ya 2050, GGML itaendelea kushiriki kikamilifu kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo miradi ya CSR ambayo inawezesha maendeleo endelevu ya Jamii zinazozunguka mgodi sambamba na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Mkuu wa mkoa wa Geita Alexander Mnyeti amemuomba mgeni rasmi, naibu waziri wa madini Dkt. Steven Kiruswa kusaidia katika utatuzi wa migogoro ya wachimbaji na wamiliki wa mashamba ambayo imekuwepo mkoani Geita

Akijibu suala hilo mgeni rasmi, naibu waziri wa madini amesema suala hilo limetolewa ufafanuzi katika sheria ya madini huku akieleza kuwa wizara itaendelea kuona namna bora ya kupokea maoni na kuboresha maeneo yenye changamoto hizo
