Storm FM

Wananchi watakiwa kufanya mazoezi kuepuka magonjwa yasiyoambukiza Geita

22 June 2026, 7:20 pm

Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Geita Herman Matemu aliyevaa njano akiwa katika picha ya pamoja kwenye Bonanza la michezo. Picha na Mrisho Sadick

Mazoezi ya mara kwa mara yana mchango mkubwa katika kupunguza hatari ya kupata magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo pamoja na unene uliopitiliza.

Na Mrisho Sadick:

Wananchi Mkoani Geita wamehimizwa kufanya mazoezi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaendelea kuwaathiri watu wengi kwa uzembe wa kutofanya mazoezi na kuzingatia lishe bora.

Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza Mkoa wa Geita Dkt. Grory Temba akizungumza kwenye bonanza la afya lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na kufanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kalangalala Manispaa ya Geita amesema magonjwa hayo yameendelea kuwa changamoto huku idadi ya wagonjwa ikiongezeka kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha usiofaa ikiwemo kutofanya mazoezi.

Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Geita Herman Matemu aliyevaa njano akiwa katika picha ya pamoja kwenye Bonanza la michezo. Picha na Mrisho Sadick

Dkt. Temba amesema mazoezi ya mara kwa mara yana mchango mkubwa katika kupunguza hatari ya kupata magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo pamoja na unene uliopitiliza, hivyo wananchi wanapaswa kuyapa kipaumbele kwa ajili ya kulinda afya zao.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Safia Jongo amewataka wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya magonjwa hayo ili kuongeza uelewa wa kukabiliana na magonjwa hayo.

Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Geita Herman Matemu aliyevaa njano akiwa katika picha ya pamoja kwenye Bonanza la michezo. Picha na Mrisho Sadick

Naye Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Geita Shafi Mwinyimvua amesema michezo na mazoezi ni nyenzo muhimu katika kuimarisha afya za wananchi ameziomba  taasisi za umma na binafsi kuendelea kuandaa mabonanza na matukio ya michezo yatakayosaidia kuhamasisha jamii kujali afya zao.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita  Herman Matemu amesema serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za utoaji elimu ya afya na kuhimiza wananchi kushiriki mazoezi mara kwa mara ili kujenga jamii yenye afya bora na nguvu kazi imara kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Baadhi ya washiriki wa bonanza hilo wameeleza kufurahishwa na tukio hilo wakisema limewapa fursa ya kufanya mazoezi, kupata elimu ya afya na kufahamu namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Katika bonanza hilo huduma mbalimbali za uchunguzi wa afya zilitolewa kwa wananchi ambapo Jumla ya watu 105 walifanyiwa upimaji wa shinikizo la damu wanaume 39 na wanawake 66 matokeo yalionyesha kuwa watu 12, wanaume 8 na wanawake 4, walibainika kuwa na shinikizo la juu la damu sawa na asilimia 12.6 ya waliopimwa, takwimu hizi zinaonesha kuwa kati ya kila watu 100 watu 13 wanaweza kuwa na tatizo la shinikizo la damu.

Aidha vijana 99 walifanyiwa upimaji wa kiwango cha sukari mwilini na hakuna hata mmoja aliyebainika kuwa na tatizo la kisukari, wakati huo huo watu 56 walifanyiwa tathmini ya uwiano wa uzito na urefu (BMI) ambapo wanaume 5 na wanawake 7, walibainika kuwa na uzito uliopitiliza , hii ni sawa na asilimia 21.4 ya waliopimwa ikimaanisha kuwa kati ya kila watu 100, takribani watu 21 wanakabiliwa na changamoto ya uzito uliopitiliza.

Kwa upande wa uchunguzi wa ugonjwa wa selimundu (sikoseli) watoto 61 walifanyiwa vipimo, kati yao watoto 9 walibainika kuwa na vinasaba vya ugonjwa huo sawa na asilimia 14.7 huku watoto 7 wakithibitika kuwa na ugonjwa wa sikoseli.

Aidha katika kuimarisha afya za watoto jumla ya watoto 167 walipatiwa matone ya Vitamini A kama sehemu ya huduma za kinga dhidi ya magonjwa na kuimarisha ukuaji wao.

Ripoti kamili na Mrisho Sasdick