

9 April 2025, 12:42 pm
“Sikujua kama ana tabia za wizi kwani alikuja kutafuta chumba cha kupanga kama wanavyofanya watu wengine na nikampa chumba” – Mwenye nyumba
Na: Amon Mwakalobo:
Binti mmoja (19) mkazi wa Nyankumbu mtaa wa Elimu kwa jina Khadija Paschal amekamatwa na Askari wa Polisi Jamii mtaa wa Msalala Road katika Manispaa ya Geita akituhumiwa kuiba vitu vya ndani vyenye thamani ya shilingi laki saba ikiwemo TV, pasi ya umeme, godoro na pesa taslimu kiasi cha shilingi laki mbili na Elfu sitini nyumbani kwa mpenzi wake maeneo ya Mitimirefu ambapo mwanaume huyo alimuacha mtuhumiwa ndani na kwenda kazini nyakati za Usiku.
Tukio hilo limetokea Jumatatu ya April 07, 2025 ambapo kwa mujibu wa mwanaume huyo Bwana Edward John amesema alimuacha nyumbani jioni akienda kazini lakini aliporudi asubuhi akakuta mlango wazi na vitu vyote vimebebwa na ndipo akatoa taarifa kwa Askari wa polisi jamii aliyemfuatilia na kumkamata maeneo ya mtaa wa Elimu, kata ya Nyankumbu alikokwenda kupanga binti huyo akiwa na vitu vyote alivyoiba.
Binti huyo amekiri kuchukua vitu hivyo na kwenda kupanga ili aanze maisha yake ambapo pesa alizoiba alitumia kupanga chumba na kumuomba mpenzi wake amsamehe asimpeleke Polisi.
Mama mwenye nyumba alipokwenda kupanga Binti huyo amesema binti huyo alifika akitafuta chumba na yeye alimpangisha bila kujua tabia zake kuwa ni mwizi.
Balozi wa shina namba 14 katika Mtaa wa Elimu Charles Sospeter amewataka wananchi wa Mtaa huo hasa wamiliki wa nyumba kuhakikisha wanatoa taarifa za wageni wote wanaowapangisha kwa viongozi wa mtaa ili kuepuka kupangisha watu wenye tabia zisizostahili.