Storm FM

Upatikanaji wa maji Nyang’hwale ni asilimia 77.4

12 December 2025, 13:55

Baadhi ya wananchi wilayani Nyang’hwale wakichota maji kwenye kituo cha maji. Picha na Mrisho Sadick

RUWASA imetakiwa kuhakikisha inapunguza upotevu wa maji na malalamiko ya bili kwa kufunga mita za wateja majumbani badala ya sehemu zilizo mbali na makazi yao.

Na Mrisho Sadick:

Hali ya upatikanaji wa maji safi na salama wilayani Nyang’hwale mkoani Geita imeendelea kuimarika na sasa imefikia asilimia 77.4 kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA ambapo kati ya vijiji 62 vya wilaya hiyo vijiji 48 ndio vinapata maji safi na salama ya uhakika.

Akizungumza katika kikao cha nusu mwaka cha wadau wa maji na vyombo vya watoa huduma ngazi ya jamii, meneja wa RUWASA wilayani Nyang’hwale Suzana Mabula amesema jitihada mbalimbali zinaendelea ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo muhimu ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 wametenga Bilioni 1.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale akizungumza kwenye kikao cha wadau wa maji. Picha na Mrisho Sadick

Amebainisha kuwa RUWASA inaendelea kutekeleza miradi mitatu mikubwa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 900, ikiwemo mradi wa visima vya Jimbo unaotekelezwa kwenye vijiji sita, mradi wa Iseni–Nyangalamila unaohusisha vijiji sita, pamoja na mradi wa maji Nyijundu nakwamba utekelezaji wa miradi hiyo unawezekana kutokana na ufadhili na msukumo wa Serikali ya Awamu ya Sita akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maji.

Sauti ya Meneja RUWASA wilaya ya Nyang’hwale

Wakati huo huo baadhi ya madiwani waliohudhuria kikao hicho wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa huduma za maji katika baadhi ya taasisi za umma licha ya maji kuwepo maeneo jirani pamoja na utofauti wa bei za kuunganisha maji majumbani jambo ambalo wamesema limekuwa kikwazo kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Nyang’hwale akizungumza baada ya kikao cha wadau wa maji kumalizika. Picha na Mrisho Sadick

Mwenyekiti wa CCM wilayani Nyang’hwale Adam Mtore ameshauri RUWASA kuhakikisha inapunguza upotevu wa maji na malalamiko ya bili kwa kufunga mita za wateja majumbani badala ya sehemu zilizo mbali na makazi yao huku Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amezitaka taasisi za serikali zilizokatiwa huduma ya maji kutokana na madeni kuhakikisha zinalipa kwa wakati ili huduma irudi haraka.

Sauti ya Mwenyekiti wa CCM na Mwenyekiti wa Halmashauri Nyang’hwale

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame ametoa onyo kali kwa baadhi ya watumishi wa umma katika Idara ya Maji wanaodaiwa kujihusisha na udanganyifu kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa wananchi amesisitiza kuwa hatavumilia kuona mwananchi akitumiwa kumfaidisha mtumishi anayependa rushwa, na akahimiza nidhamu na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za maji wilayani humo.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale
Wadau wa maji mbalimbali wakiwa kwenye kikao wilayani Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Wilaya ya Nyang’hwale ina jumla ya Vijiji 62 vyenye wakazi 225,803 kwa Mujibu wa Sensa na Makazi ya mwaka 2022 vinavyopata huduma ya maji safi na salama ni vijiji 48 huku jumla ya wakazi 174,772 kati ya 225,803 ndiyo wanaopata huduma ya Maji safi na salama.