Storm FM

Mimba za utotoni zawaibua wananchi kujenga shule, RC Geita akagua nakutoa maagizo

23 June 2026, 5:49 pm

Wakazi wa Kijiji cha Ndelema wakiwa kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa Kijijini humo. Picha na Mrisho Sadick

Mimba za utotoni nakutembea umbali mrefu wanafunzi hususani wa kike kwenda katika shule ya sekondari Kamena zawaibua wananchi wa Ndelema kujenga shule yao

Na Mrisho Sadick:

Hofu ya kuongezeka kwa mimba za utotoni miongoni mwa wanafunzi wa kike katika Kata ya Kamena Halmashauri ya wilaya ya Geita Mkoani Geita imewalazimu wananchi wa Kijiji cha Ndelema kuanzisha ujenzi wa shule yao ya sekondari ili kuwaondolea changamoto watoto wao ya kutembea umbali mrefu kwenda katika Shule ya Sekondari Kamena.

Mtendaji wa Kata ya Kamena Joseph Emmanuel akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita wakati wa ukaguzi wa mradi huo amesema wananchi kwa kushirikiana na wahisani na Serikali Kuu wamefanikiwa kuchangia zaidi ya shilingi milioni 46 zilizowezesha ujenzi wa madarasa mawili yaliyokamilika na darasa moja linaloendelea kukamilishwa huku.

Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa shule ya Sekondari Ndelema. Picha na Mrisho Sadick

Hata hivyo, shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyoo, jengo la utawala na nyumba za walimu , Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba amepongeza jitihada za wananchi za kuanzisha ujenzi huo huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Safia Jongo akitoa wito wa mapambano dhidi ya mimba za utotoni zinazokatisha ndoto za wanafunzi wengi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita akizungumza katika ziara ya mkuu wa mkoa wa Geita katika kijiji cha Ndelema. Picha na Mrisho Sadick

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema katika mwaka fedha ujao serikali itatoa shilingi milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na vyoo ili kuwezesha Shule ya Sekondari Ndelema kuanza kupokea wanafunzi na kupunguza changamoto zinazowakabili watoto wa eneo hilo.

Ripoti kamili ya Stori hii na Mrisho Sadick