Storm FM

Wanawake kujifungulia njiani kumewasukuma kuanzisha Zahanati

21 February 2024, 12:20 am

Wakazi wa Bwenda wakiwa katika mkutano wa Kamati ya siasa ya CCM Katika Zahanati waliyoijenga. Picha na Mrisho Sadick

Changamoto ya vifo vya kina mama wajawazito na watoto kufariki njiani bado ni tatizo ambapo baadhi ya watu wameendelea kutafuta ufumbuzi kwa kusogeza huduma za afya karibu na makazi yao.

Na Mrisho Sadick:

Wakazi wa Kitongoji cha Bwenda Kata ya Katente wilayani Bukombe Mkoani Geita wameungana kwa pamoja kuanzisha ujenzi wa Zahanati katika eneo hilo ili kuondokana na changamoto ya wanawake kujifungulia njiani wakati wakifuata huduma za afya Hospitali ya wilaya hiyo.

Mafundi wakiendelea na ujenzi katika Zahanati ya Bwenda. Picha na Mrisho Sadick

Wakizungumzia hatua hiyo baadhi ya wakazi wa Kitongoji hicho baada ya kutembelewa na Kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita wamesema wameamua kuanzisha ujenzi wa Zahanati hiyo ili kuondokana na changamoto nyingi ikiwemo kuokoa vifo vya akina mama na watoto.

Sauti ya wananchi wa Bwenda
Kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Geita ikiwa katika ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mkuu wa wilaya ya Bukombe Said Nkumba amewapongeza wananchi wa kitongoji hicho kwa kujitoa kuanzisha ujenzi wa zahanati ambapo baada ya hatua hiyo serikali iliwaunga mkono kwa kuwapatia milioni 50 huku Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt Omari Sukari akisema atahakikisha inapata usajili nakuanza kutoa huduma rasmi licha ya huduma za kliniki kuanza kutolewa.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Bukombe na Mganga Mkuu wa Mkoa

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema  Mkoa wa Geita umepokea milioni 550 kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati 11 ikiwemo ya Kitongoji hicho Cha Bwenda nakuwahakikishia Wananchi kuwa itaanza kutoa huduma.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Geita

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila amewashukia baadhi ya watu waliyokuwa wakibeza Juhudi za ujenzi wa Zahanati hiyo nakuwaahidi kuwa atafuatilia kuhakikisha inaanza kutoa huduma haraka.

Sauti ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita