Storm FM

Sita wafariki ajali ya gari Bukombe

13 July 2023, 2:59 pm

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita ACP Safia Jongo. Picha na Mrisho Sadick

Usingizi wa dereva wa gari dogo la abiria Toyota Hiace umekatisha uhai wa watu sita katika kata ya Runzewe wilayani Bukombe mkoani Geita.

Na Mrisho Sadick:

Watu sita wamefariki dunia na wawili kujeruhiwa baada ya gari dogo aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T769 DQP kugongana uso kwa uso na lori la mizigo katika kata ya Runzewe wilayani Bukombe mkoani Geita.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Safia Jongo akizungumza na Storm FM kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba limetokea majira ya saa 12:00 asubuhi leo huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni dereva wa Hiace kusinzia wakati akiwa mwendo kasi na kugongana na lori la mizigo.

Amesema miongoni mwa watu waliofariki katika ajali hiyo ni dereva wa Hiace na kwamba majeruhi hao wawili wamefikishwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita kwa uangalizi zaidi huku akitoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Sauti ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita ACP Jongo