Storm FM

Kicheko kwa bodaboda Storm Fm ikisaidia kutatua changamoto yao

10 July 2023, 8:42 pm

Waendesha pikipiki wakiwa kwenye egesho Nyankumbu. Picha na Kale Chongela.

Kutokana na changamoto ya muda mrefu ya kutozwa faini iliyokuwa ikiwasumbua waendesha pikipiki katika soko la Nyankumbu mjini Geita hatimaye adha hiyo imetatuliwa baada ya Storm FM kufika na kuripoti changamoto hiyo.

Na Kale Chongela

Waendesha pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda katika soko la asubuhi lililopo kata ya Nyankumbu halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita wamekipongeza kituo cha Storm FM kwa kusaidia kutatua changamoto ya baadhi yao kutozwa faini kinyume na utaratibu.

Changamoto hiyo iliripotiwa kwa mara ya kwanza miezi mitatu iliyopita kwa waendesha pikipiki hao kuwalalamikia watu wanaodaiwa kuwa ni Polisi Jamii wa mtaa huo, kuwakamata na kuwatoza faini wanapokuwa wameegesha vyombo vyao vya usafiri kwenye soko hilo, kwa madai kuwa ni kinyume cha utaratibu.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Enos Chelehan alipofikiwa na kituo hiki wakati huo alikanusha madai hayo kuwa ofisi yake haijatuma watu kuchukua faini kwa waendesha bodaboda wanapofanya makosa na akaahidi kulifuatilia suala hilo na kuchukua hatua za haraka.

Wakizungumza na Storm FM kwa furaha, baadhi ya waendesha pikipiki hao wamesema tangu suala hilo liripotiwe watu hao hawajaonekana tena eneo hilo hali ambayo imewaongezea ari ya kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa hapo awali walikuwa wakikumbana na faini hadi shilingi elfu kumi na hawajui inapelekwa wapi.