Storm FM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awaondoa hofu wananchi

27 March 2021, 3:26 pm

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa baada ya mazishi ya Dkt. John Magufuli , kinachofuata ni utekelezaji wa ahadi zote ambazo yeye na chama chake (Chama cha Mapinduzi) waliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Rais Samia amesema hayo jana wilayani Chato mkoani Geita wakati akitoa salamu za pole kwa familia ya Dkt Magufuli na waombolezaji wengine waliofika kwenye Misa Takatifu ya mazishi ya kiongozi huyo.

Amesema kuwa Tanzania imempoteza Jemedari, lakini watendaji na wasaidizi aliokuwa akifanya nao kazi bado wapo hivyo watatekeleza yale yote aliyoahidi kwa wananchi.

Kuhusu ahadi ya kuifanya wilaya ya Chato kuwa mkoa ambayo Dkt. Magufuli alikuwa ameahidi, Rais Samia amesema kuwa anafahamu kwamba mchakato wa hilo umeanza na amewataka watendaji kuendelea nao, na kwamba wataangalia kama vigezo vimetimia.