Storm FM

Miti 3,000 kupandwa Geita maadhimisho ya miaka 40 ya NEMC

15 May 2026, 4:52 pm

Mgeni rasmi Dkt. Elfas Msenya akipanda miti katika chuo cha VETA Geita. Picha na Ester Mabula

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) lilianzishwa mwaka 1986 ambapo maadhimisho ya miaka 40 yanatarajiwa kufanyika Mei 30, 2026.

Na: Ester Mabula

Kuelekea maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC), Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi imezindua kampeni ya upandaji miti zaidi ya 3,000 katika Mkoa wa Geita huku zaidi ya miti 40,000 ikitarajiwa kupandwa nchi nzima kama sehemu ya juhudi za utunzaji wa mazingira.

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lililofanyika leo Mei 15, 2026 katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Geita, Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi, Mhandisi Boniphace Guni amesema tangu NEMC ianzishwe mwaka 1986 imeendelea kusimamia jukumu lake la msingi la kuratibu na kusimamia mazingira nchini.

Sauti ya Eng. Boniphace Guni, Meneja NEMC
Meneja wa NEMC Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi, Eng. Boniphace Guni akitoa taarifa mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani). Picha na Ester Mabula

Mgeni rasmi katika hafla hiyo Dkt. Elfas Msenya kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Geita ameipongeza NEMC kwa kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira akieleza serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zote za utunzaji wa mazingira.

Sauti ya Dkt. Elfas Msenya, mgeni rasmi
Mgeni rasmi Dkt. Elfas Msenya akizungumza kuelekea miaka 40 ya NEMC. Picha na Ester Mabula

Katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira mkoani Geita Kampuni ya Geita Gold Minning Limited (GGML) imeendelea kushirikiana na serikali pamoja na NEMC ambapo akizungumza Meneja wa mazingira kutoka GGML Bw. Mhando Yusuph amesema wanaamini katika kutunza mazingira kupitia sera zinazoongoza shughuli za mgodi huo.

Sauti Mhando Yusuph kutoka GGML

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Geita Sebastian Masigo amesema chuo hicho kimeendelea uzingatia kanuni bora za uhifadhi mazingira huku wanachuo wakipongeza hatua hiyo kuwa italeta tija pamoja na kuboresha mazingira ya chuo.

Sauti ya kaimu mkuu wa chuo na wanachuo
Mhando Yusuph kutoka kampuni ya GGML akipanda mti katika chuo cha VETA Geita. Picha na Ester Mabula