Storm FM
Storm FM
11 June 2026, 4:02 pm

Washiriki wa mafunzo hayo ni kutoka mikoa ya Geita , Dar es salaam, Mwanza , Ruvuma, Dodoma , Njombe , Mbeya na mikoa mingine ya Tanzania wamechangamkia fursa hiyo.
Na Mrisho Sadick:
Mjumbe wa Kamati tendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Kanda ya Tano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA) Salum Kulunge amewataka wahitimu wa Kozi ya Ukocha wa Makipa ya Diploma D ngazi ya awali kutumia elimu waliyoipata kukuza mchezo wa soka nchini.
Kulunge ametoa kauli hiyo wakati akifunga rasmi kozi hiyo ya awali iliyofanyika kwa mara ya kwanza nje ya makao makuu ya TFF, huku Mkoa wa Geita ukiandika historia kwa kuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza kupata fursa hiyo amewataka makocha hao kutojihusisha na vitendo visivyokubalika michezoni ikiwemo vya ubashiri na upangaji wa matokeo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Geita (GEDFA) Ally Twist amewataka wahitimu hao kwenda kutumia ujuzi walioupata kusaidia kutatua changamoto ya uhaba wa makipa wazawa inayolikabili soka la Tanzania.
Katibu wa GEDFA Shafii Mwinyimvua amesema washiriki 20 kutoka mikoa mbalimbali nchini wameshiriki mafunzo hayo ya siku tano yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Kisesa Manispaa ya Geita huku miongoni mwa washiriki hao ni wachezaji wa zamani wa vilabu mbalimbali ikiwemo Simba na Yanga.

Naye mkufunzi wa kozi hiyo Josia Kasasi amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa TFF wa kuimarisha idara ya makipa kwa kuzalisha makocha wengi zaidi watakaosaidia kuibua na kuendeleza vipaji vya makipa nchini huku baadhi ya washiriki wakiipongeza TFF kwa hatua hiyo.