Storm FM
Storm FM
12 July 2026, 8:12 pm

Kukamilika kwa Kituo cha Afya Rwamgasa kunatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, na kupunguza gharama pamoja na muda ambao wananchi walikuwa wakitumia kufuata huduma katika maeneo ya mbali.
Na Mrisho Sadick:
Wananchi wa Kata ya Rwamgasa Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani Geita wanatarajia kuondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Rwamgasa kilichojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 900.
Kata hiyo yenye idadi kubwa ya wakazi kutokana na shughuli za uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya licha ya kuwepo kwa zahanati baadhi ya wananchi wanalazimika kusafiri hadi Kituo cha Afya Katoro kupata matibabu hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu mkubwa na wakati mwingine kuhatarisha maisha yao.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo na kueleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa pamoja na ubora wa kazi zilizotekelezwa, wajumbe wa kamati hiyo pia wamewataka wananchi kulinda miundombinu hiyo ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila ameagiza kituo hicho kianze mara moja kutoa huduma kwa wananchi nakwamba kutokana na Wilaya ya Geita kuwa na majimbo manne huku matatu tayari yakiwa na hospitali zenye hadhi ya wilaya kuna mpango wa kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Rwamgasa kuwa hospitali katika siku zijazo ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma za afya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema hadi sasa gharama za ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho zinakaribia kufikia shilingi bilioni moja jambo linaloonesha dhamira ya serikali ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kamati hiyo ilipokuwa kwenye ziara hiyo pia ilipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu kupitia Programu ya Tanzania Maternal and Child Health Investment Program (TMCHIP) ikiwemo ujenzi wa jengo pacha la upasuaji wodi na maabara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Geita ilipokea shilingi milioni 459,929,407 tarehe 5 Mei 2025 kwa ajili ya ujenzi wa majengo katika Kituo cha Afya Rwamgasa kupitia akaunti ya Zahanati ya Rwamgasa, Ujenzi ulianza rasmi tarehe 5 Desemba 2025 na kukamilika tarehe 30 Juni 2026.
Katika matumizi ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 370,577,540 kimelipwa kwa wazabuni wa vifaa na malighafi za ujenzi, huku mafundi wakilipwa shilingi milioni 89,500,000 na kufanya jumla ya shilingi milioni 460,077,540 zilizotumika katika utekelezaji wa mradi huo.