Storm FM

Ujenzi wa kituo cha afya Busolwa uko hatua nzuri

4 June 2026, 3:55 pm

Muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa majengo ya kituo cha afya Busolwa. Picha na Mrisho Sadick

Kukamilika kwa Kituo hicho cha Afya kunatarajiwa kuwaondolea changamoto wananchi kwenda katika Vijiji vya Kharumwa, Nyankurukuru na Kagunga kutafuta huduma za ngazi ya Kituo Cha Afya.

Na Mrisho Sadick:

Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya Wilayani Nyang’hwale mkoani Geita baada ya kutoa Shilingi Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Busolwa, mradi unaotarajiwa kuondoa changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Afya vijiji jirani.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Busolwa Zacharia Chacha amesema Serikali imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la wazazi, kichomea taka na vyoo.

Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale akizungumza katika ziara ya mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame amesema fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na michango kutoka kwa wadau mbalimbali zimekuwa zikisimamiwa na kutumika kwa ufanisi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema kuwa mara baada ya kituo hicho kukamilika na kuanza kutoa huduma Serikali itapeleka vifaa tiba muhimu pamoja na watumishi wa afya ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi.

Mkuu wa mkoa wa Geita akizungumza na wnanchi katika ujenzi wa kituo cha afya Busolwa. Picha na Mrisho Sadick

Ripoti kamili ya Stori hii na Mrisho Sadick