Storm FM

DC Kingalame akabidhi madawati zaidi ya 1,000 Nyangh’wale

4 June 2026, 1:28 pm

Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela aliyeketi katikati akiwa katika hafla ya kupokea na kukabidhi madawati. Picha na Mrisho Sadick

Madawati hayo yanatarajiwa kuanza kusambazwa mara moja katika shule za sekondari zilizoathirika zaidi na upungufu huo, hatua inayotarajiwa kuboresha mazingira ya ufundishaji.

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita Grace Kingalame amekabidhi zaidi ya madawati 1,000 kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati katika shule za sekondari wilayani humo.

Hatua hiyo imekuja baada ya DC Kingalame kufanya ziara katika shule mbalimbali za sekondari mwezi Desemba mwaka jana na kubaini uwepo wa upungufu wa madawati hali iliyokuwa ikiathiri mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Mkuu wa wilaya ya Nyangh’wale kulia akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Geita Madawati zaidi ya 1,000. Picha na Mrisho Sadick

Baada ya kubaini changamoto hiyo Kingalame kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Nyang’hwale walichukua hatua za kutafuta wadau mbalimbali ili kusaidia kupunguza tatizo hilo juhudi hizo zimezaa matunda baada ya kupatikana kwa madawati zaidi ya 1,000 ambayo sasa yanatarajiwa kusambazwa katika shule za sekondari zenye uhitaji mkubwa.

Sauti ya DC Kingalame

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea madawati hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amepongeza uongozi wa Wilaya ya Nyang’hwale kwa ubunifu na juhudi walizoonyesha katika kutatua changamoto hiyo muhimu ya elimu.

Shigela amesema hatua hiyo ni mfano mzuri wa namna viongozi wanavyoweza kushirikiana na wadau wa maendeleo kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Geita
Mkuu wa Mkoa wa Geita kushoto akimkabidhi Mkurugenzi wa Nyangh’hwale Madawati. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale amesema kupatikana kwa madawati hayo kutapunguza kwa kiwango kikubwa changamoto iliyokuwa ikiikabili halmashauri hiyo huku akibainisha kuwa juhudi zaidi zinaendelea kufanyika ili kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa madawati katika shule zote za sekondari.

Sauti ya Mkurugenzi Nyangh’wale