Storm FM
Storm FM
6 July 2026, 7:59 pm

Kufuatia kusambaa kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii juu ya kufanyika kwa maandamano nchini CCM imeendelea kuwataka kupuuza taarifa hizo zenye lengo la kuvuruga amani.
Na Mrisho Sadick:
Katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Geita Andrew Mnunke amewataka wakazi wa Mkoa wa Geita kuendelea kudumisha amani na utulivu huku wakipuuza taarifa zinazochochea uvunjifu wa amani katika mitandao ya kijamii.
Mnunke ametoa wito huo hivi karibuni wakati wa hafla ya kuipongeza timu ya Geita Gold FC kufuatia kufanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Tanzania Bara, amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa hivyo kila mwananchi ana jukumu la kuhakikisha inalindwa kwa kauli na vitendo.
Amesisitiza kuwa baadhi ya taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zina lengo la kupotosha wananchi na kuvuruga mshikamano hivyo amewahimiza wakazi wa Geita kuendelea kuwa watulivu, kuamini vyombo husika na kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji.
Aidha Mnunke ameipongeza Geita Gold FC kwa mafanikio ya kurejea Ligi Kuu ya Tanzania Bara, akieleza kuwa ushindi huo ni fahari kwa Mkoa wa Geita na matokeo ya juhudi za viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wa timu hiyo.