Storm FM
Storm FM
29 June 2026, 5:07 pm

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeshiriki hafla ya utoaji wa Tuzo za Business SDG Awards 2026 kama mdhamini wa ngazi ya Dhahabu (Gold Sponsor), ikiungana na viongozi waandamizi wa Serikali na sekta binafsi.
Na: Ester Mabula
Hafla hiyo imefanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.iliandaliwa na Global Compact Network Tanzania (GCNT) kwa lengo la kutambua mchango wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
Tuzo hizo, ambazo zimefanyika kwa mwaka wa nne mfululizo, zimeendelea kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha viongozi wa biashara, watunga sera, mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wa maendeleo ili kutambua kampuni zinazotekeleza kwa vitendo Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo muhimili mkuu wa kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa lengo la Tanzania kuwa na uchumi wa dola trilioni moja za Marekani haliwezi kufikiwa bila mchango mkubwa wa wawekezaji na wafanyabiashara.
Aliongeza kuwa tangu mwanzo wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo 2050, sekta binafsi imepewa nafasi ya kipekee katika kuongoza ukuaji wa uchumi.
GGML iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Uendelevu na Ushirikishwaji wa Wadau, Bw. Simon Shayo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya GCNT Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Shayo amesema dhana ya maendeleo yanayoweka wananchi mbele imekuwa sehemu ya falsafa ya maendeleo ya Tanzania tangu kipindi cha uhuru.
Aidha, ametambua juhudi za Serikali katika kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, akibainisha kuwa sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) pamoja na maboresho ya mazingira ya biashara vinaonesha dhamira ya Serikali ya kutambua mchango wa wadau wasiokuwa wa Serikali katika maendeleo ya taifa.
Udhamini wa GGML katika ngazi ya Dhahabu unaonesha dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono shughuli za GCNT pamoja na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Kwa zaidi ya miaka 25 ya shughuli zake katika Mkoa wa Geita, GGML imeajiri zaidi ya watu 7,000, ambapo asilimia 98 ni Watanzania. Katika kipindi hicho, kampuni hiyo imechangia zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.7 kama mapato ya kodi kwa Serikali ya Tanzania, sambamba na kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira na ukuaji wa uchumi wa taifa.