

11 June 2025, 2:05 pm
Wafanyabiashara waangua kilio wakidai kupoteza mamilioni ya pesa baada ya maduka yao kuteketea kwa moto usiku.
Na Mrisho Sadick:
Moto ambao chanzo chake bado hakijajulikana umeteketeza maduka 17 pamoja na stoo zake usiku wa june 10,2025 katika Kata ya Buseresere wilayani Chato Mkoani Geita.
Tukio hilo limetokea majira ya saa tatu usiku wa Juni 10 mwaka huu , ambapo juhudi za kuuzima moto huo zilichelewa kutokana na kutokuwepo kwa gari la zimamoto katika eneo pamoja na wahusika kuchelewa kutoa taarifa kwa Jeshi la zimamoto na uokoaji huku wamiliki wa maduka hayo wakilia kupata hasara ya mamilioni fedha.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Buseresere Kasezero Athuman akizungumza kwenye eneo la tukio amesema moto huo ulianza kuwaka ndani ya duka ambalo mchana kulikua na shughuli za uchomeleaji wa geti nahuenda ndio kikawa chanzo Cha moto huo.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Geita Shabaani Dawa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa walipata taarifa rasmi saa nne kasoro usiku licha ya moto huo kuanza kuwaka saa mbili na nusu huku akiwataka wananchi kutoa taarifa haraka pindi tu wanapohisi hatari ya moto.