Storm FM

Vikundi 21 vyakopeshwa milioni 162 Nyang’hwale

1 May 2026, 7:42 pm

Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale akikabidhi mfano wa hundi ya mkopo wa asilimia 10 kwa vikundi. Picha na Mrisho Sadick

Katika mwaka wa fedha 2025/2026 Nyang’hwale imetenga zaidi ya shilingi milioni 396 kwa ajili ya mikopo hiyo, ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 280 tayari zimeshatolewa, sawa na zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji

Na Mrisho Sadick:

Serikali wilayani Nyanghwale mkoani Geita imewataka maafisa maendeleo na watendaji wa kata kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kuunda vikundi ili kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa kuwa ni haki yao ya msingi.

Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale Bi. Grace Kingalame katika hafla ya kukabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 162 kwa vikundi 21 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Msalala, kata ya Kharumwa.

Mkuu wa Wilaya ya Nyanghwale Bi. Grace Kingalame akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo. Picha na Mrisho Sadick

Katibu tawala wa wilaya ya Nyang’hwale Kaunga Amani na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo John Isack wameendelea kusisitiza suala la uwajibikaji wa watendaji ngazi ya Kata kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa juu ya mikopo hiyo ili kila mtu hususani wanawake wawe na uwezo wa kujitokeza kuomba mikopo bila woga.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 wilayani Nyang’hwale wakiwa katika hafla ya utoaji wa mikopo. Picha na Mrisho Sadick

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Majagi Maiga amesema wataendelea kusimamia na kulea vikundi vinavyopata mikopo ili kuhakikisha inatumika kama ilivyokusudiwa, huku afisa maendeleo ya jamii wilayani humo Yahaya Selemani amesema kati ya vikundi 21 vilivyopata mikopo hiyo yenye jumla ya shilingi milioni 162, vikundi 7 vya wanawake vimepatiwa shilingi milioni 53, vikundi 10 vya vijana vikipata shilingi milioni 92, huku vikundi 4 vya watu wenye ulemavu vikipewa shilingi milioni 17.

Mratibu wa mikopo ambae ni afisa maendeleo ya jamii wilayani Nyang’hwale Yahaya Selemani akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo. Picha na Mrisho Sadick

Aidha, kati ya vikundi 56 vilivyoomba mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 932, ni vikundi 21 pekee vilivyokidhi vigezo na kufanikiwa kupatiwa mkopo huo huku vikundi ambavyo havikufanikiwa vitaendelea kujengewa uwezo ili viweze kunufaika katika awamu zijazo.

Ripoti kamili ya stori hii na Mrisho Sadick