Storm FM

TAKUKURU Geita yakutana na wadau wa maendeleo Geita

3 July 2026, 1:04 pm

Mkuu wa TAKUKURU Geita Ndg. James Ruge akizungumza katika warsha iliyofanyika Julai 02, 2026. Picha na Ester Mabula

“Uwepo wa warsha hii ni miongoni mwa mikakati ya TAKUKURU katika kuimarisha ushirikiano na watekelezaji pamoja na wasimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya Rushwa inayorudisha nyuma maendeleo” – James Ruge

Na: Ester Mabula

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita Ndg. James Ruge, amesema uzoefu unaonyesha bado kuna changamoto katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo kutofuata sheria, usimamizi dhaifu wa mikataba, ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi, malipo yasiyostahili pamoja na migongano ya maslahi inayochangia upotevu wa fedha za umma na kushindwa kufikiwa kwa malengo ya miradi ya maendeleo yaliyokusudiwa.

Ameeleza hayo Julai 02, 2026 katika warsha iloyoandaliwa na TAKUKURU ikihusisha wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoa wa Geita.

Mkuu wa Takukuru James Ruge amesema changamoto zinazojitokeza zinaweza kupunguzwa kwa kuwashirikisha wadau wote katika utekelezaji wa miradi, kuhakikisha uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma sambamba na kuongeza uwajibikaji ili kurekebisha kasoro zinazobainika katika miradi mbalimbali.

Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela akizungumza katika warsha iliyoandaliwa na TAKUKURU. Picha na Ester Mabula

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela ambaye alikuwa mgeni rasmi,  amesema juhudi zinazofanywa na TAKUKURU katika kuzuia rushwa zimekuwa na mchango mkubwa, hususani kupitia ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kubaini na kuziba mianya ya rushwa kabla haijaleta athari.

Baadhi ya washiriki kutoka idara mbalimbali ambao wameshiriki katika warsha hiyo wametoa maoni yao ili kuboresha utendaji kazi wa TAKUKURU sambamba na kuchochea maendeleo huku Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila akiwataka watendaji wa serikali kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na stahiki.

Sauti ya Ester Mabula ikieleza zaidi
Baadhi ya wadau wa maendeleo walioshiriki katika warsha hiyo iliyoandaliwa na TAKUKURU Geita. Picha na Ester Mabula