Storm FM

Serikali ya mtaa yaonya wahalifu kutumia maboma Geita

10 August 2026, 12:33 pm

Inadaiwa kuwa baadhi ya watu wanatumia maboma hayo kuratibu na kupanga matukio ya uhalifu nakwamba ni hatari kwa usalama wa mali na maisha ya watu.

Na Kale Chongela:

Serikali ya Mtaa wa Mkoani Kata ya Kalangalala Manispaa ya Geita imewataka wamiliki wa nyumba ambazo bado hazijakamilika kuhakikisha wanakamilisha au kuweka milango kwenye maboma hayo ili kuzuia wahalifu kuyatumia kama sehemu za kujificha , kuratibu na kupanga vitendo vya uhalifu.

Akizungumza na Storm FM Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkoani Bw. Salvatory Daniel Paul amesema kuwa maboma mengi ambayo hayajawekewa milango yamekuwa yakitumiwa na watu wasiojulikana hali ambayo imekuwa ikichangia ongezeko la matukio ya wizi na kuhatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo.

Aidha Bw. Salvatory amesema kuwa mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama katika mtaa huo inaendelea kutekelezwa huku akisisitiza kuwa suala la usalama wa jamii ni jukumu la kila mwananchi na linahitaji ushirikiano wa pamoja.

Sauti ya Mwenyekiti wa mtaa wa Mkoani

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamewataka wamiliki wa nyumba ambazo hazijakamilika kuchukua hatua za haraka za kuweka milango, wakieleza kuwa baadhi ya maboma hayo yamekuwa yakitumika kama maficho ya watu wasiojulikana na hivyo kuhatarisha usalama wa jamii.

Sauti ya wananchi mtaa wa Mkoani