Storm FM
Storm FM
10 September 2026, 2:57 pm

Mwili wa Lucas Tanganyika umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema wakati taratibu za mazishi zikiendelea.
Na Mrisho Sadick:
Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Lucas Tanganyika (56) mkazi wa Kitongoji cha Ikelege Kata ya Sima Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza amefariki dunia kwa madai ya kujinyonga hadi kufa ndani ya nyumba yake huku chanzo cha tukio hilo kikiwa hakijulikani.
Tukio hilo limetokea septemba 9,2026 Nyumbani kwa marehemu ambapo watoto na majirani wa familia hiyo wamesema hawajui nini kimemkuta Tanganyika hadi kufikia kuchukua maamuzi hayo magumu nakwamba walimkuta ndani katika chumba chake akiwa amejinyonga.
Wananchi wametumia kisa hicho kutoa wito kwa watu wengine wanaokabiliwa na changamoto na maisha kuwashirikisha watu wengine matatizo yao ili kuona namna ya kuyatatua nasiyo kuchukua maamuzi magumu kama hayo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikelege Ezekiel Merick amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa limetokea majira ya saa nne asubuhi amesema marehemu alikutwa akiwa ndani ya nyumba yake katika hali hiyo na taarifa zilitolewa kwa mamlaka husika.
Baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi Wilaya ya Sengerema lilifika katika eneo la tukio kwa ajili ya taratibu za kisheria kisha waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya taratibu zaidi.