Storm FM

Mbunge atoa kompyuta 5 Ihanamilo sekondari

9 March 2025, 2:45 pm

Mbunge Kanyasu akiwa katika zoezi la kukabidhi kompyuta za kisasa kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Ihanamilo. Picha na Mrisho Shabani.

Wadau mbalimbali wa elimu wameombwa kuendelea kujitokeza kusaidia sekta hiyo hususani katika masuala ya TEHAMA.

Na Mrisho Shabani:

Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Costantine Kanyasu ametoa Kompyuta  zenye thamani ya zaidi ya milioni 10 katika shule ya sekondari Ihanamilo Manispaa ya Geita Mkoani Geita ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Naibu Waziri Mkuu Dkt Doto Biteko aliyoitoa wakati wa ziara yake katika Kata hiyo.

Zoezi la kukabidhi Komputa hizo tano za kisasa limefanyika katika shule ya sekondari ya Ihanamilo Manispaa ya Geita nakuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wananchi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo ambapo Mhe Kanyasu amesema ametoa vifaa hivyo ikiwa ni sehemu ya ahadi ya naibu waziri mkuu Dkt Doto Biteko.

Sauti ya Mbunge Kanyasu
Wanafunzi wa shule ya sekondari Ihanamilo wakiwa katika zoezi la kukabidhiwa kompyuta na Mbunge wa Jimbo la Geita mjini. Picha na Mrisho Shabani.

Awali Diwani wa Kata ya Ihanamilo Joseph Lugaila na mkuu wa shule hiyo Salum mkumalila wamempongeza mbunge kanyasu kwa kutimiza ahadi hiyo waliyoiomba kwa muda mrefu kwa Naibu Waziri Mkuu.

Sauti ya diwani na Mkuu wa shule
Wananchi , wazazi na walezi wakiwa katika sekondari ya Ihanamilo katika zoezi la kukabidhiwa kompyuta na Mbunge wa Jimbo la Geita mjini. Picha na Mrisho Shabani.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Ihanamilo wamemshukuru mbunge kwa kutimiza ahadi hiyo huku wakiipongeza serikali kwa kufikisha nishati ya umeme katika eneo hilo hali ambayo imeongeza ari ya wanafunzi kujifunza wakati wote.