

14 June 2025, 10:38 am
Licha ya serikali kuendelea kuwatangazia wananchi waliosajiliwa kwenda kuchukua vitambulisho vyao lakini bado kuna idadi kubwa ya watu hususani vijijini wanadai kutosajiliwa.
Na Mrisho Sadick:
Wakazi wa kijiji cha Nyakagomba Halmashauri ya wilaya ya Geita Mkoani Geita wameiomba serikali kuwapelekea huduma ya usajili wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwakuwa idadi kubwa ya wakazi wa Kijiji hicho hususani vijana hawana vitambulisho hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kijiji hicho mbele ya mkuu wa mkoa wa Geita Juni 12,2025 Mzee Revocatus Ernest amesema waathirika wa kwanza wa changamoto hiyo ni vijana kwakuwa wanakosa fursa nyingi ikiwemo ajira kwasababu yakutokuwa na vitambulisho vya Taifa NIDA.
Meneja wa NIDA Mkoa wa Geita Ramadhani Charles mesema kabla ya mwaka huu wa Fedha kuisha mamlaka hiyo itafika katika kijiji hicho kwa ajili ya kuwasajili na kuwatambua wananchi ambao hawana vitambulisho hivyo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amewatoa hofu Wananchi kuhusu usajili huo kwakuwa serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya zoezi hilo nakwamba kabla ya mwezi Juni kuisha maafisa wa NIDA watafika kwenye Kijiji hicho kwa ajili ya kuwatambua nakuwasajili.