Storm FM

Wamiliki nyumba za wageni waja juu tozo ya kitanda

5 July 2023, 3:47 pm

Wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni mkoani Geita kwenye mkutano mkuu wa umoja huo. Picha na Mrisho Sadick

Kufuatia uchukuaji tozo ya asilimia moja kwa kila kitanda kwenye nyumba za kulala wageni mkoani Geita, wafanyabiashara wa nyumba hizo wameamua kusimama kidete ili serikali ipitia upya na kutoa muongozo wa tozo hizo.

Na Mrisho Sadick -Geita

Umoja wa Wafanyabiashara wa Nyumba za kulala wageni mkoani Geita wameiomba serikali kupitia upya na kutoa muongozo wa tozo ya asilimia moja kwa kila kitanda kwani bado inaleta mkanganyiko.

Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara hao, Seleman Maganga akizungumza kwenye mkutano mkuu wa umoja huo amesema tangu mwezi januari mwaka huu walipewa maelekezo ya kulipa tozo hiyo kwa barua kutoka Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kuwa wahusika wa tozo hiyo ni wamiliki wa nyumba za kulala wageni waliyochapishwa kwenye gazeti la serikali na zikatangazwa bila wao kujua.

Sauti ya Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara Seleman Maganga

Katibu wa Umoja wa wafanyabiashara hao, Makelele Zunzu amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya wao kukosa ufafanuzi kutoka kwa mamlaka husika kwani mara zote wanapohoji juu ya tozo hiyo hawapati majibu.

Sauti ya Katibu wa Umoja wa wafanyabiashara Makelele Zunzu
Jengo la ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick.

Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa Geita, Maimuna Khatibu amesema Kodi hiyo inalipwa kwa mjibu wa sheria ya utalii ya mwaka 2008 na kanuni za mwaka 2013 na kuwataka wafanyabiashara hao kuendelea kutekeleza wajibu wa kulipa asilimia moja ya gharama ya kitanda kwani ipo kwa mjibu wa sheria.

Sauti ya Kaimu Meneja wa TRA mkoa wa Geita, Maimuna Khatibu