Storm FM

Wakulima Chato kunufaika na kilimo cha umwagiliaji

13 July 2023, 9:59 am

Wananchi Chato wakiwa katika uzinduzi wa kampeni ya mapinduzi ya kilimo. Picha na Mrisho Sadick

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi kusababisha kupungua kwa mvua wilayani Chato mkoani Geita, serikali imekuja na njia mbadala ya kilimo cha umwagiliaji ili kuwakomboa wakulima.

Na Mrisho Sadick:

Serikali imepanga kuboresha mifumo ya umwagiliaji kwa wakulima wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria  wilayani Chato mkoani Geita ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yamechangia kupungua kwa mvua wilayani humo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde katika uzinduzi wa kampeni ya mapinduzi ya kilimo na uchumi wilayani Chato, ambapo amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekipa kilimo kipaumbele kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 miaka miwili iliyopita hadi kufikia bilioni 970 mwaka 2023/2024.

Naibu Waziri wa Kilimo Antony Mavunde akiwa na viongozi mbalimbali akizindua kampeni ya mapinduzi ya kilimo Chato. Picha na Mrisho Sadick
Sauti ya Naibu Waziri wa Kilimo Antony Mavunde

Mkuu wa wilaya ya Chato Deusdedit Katwale amesema lengo la uzinduzi huo ni mabadiliko ya kifikra , mtazamo , mwenendo,utamaduni na mifumo iliyozoeleka kutumika katika uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kumkomboa mkulima kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Sauti ya Mkuu wa wilaya Chato Deusdedit Katwale

Kwa upande wake  Mbunge wa jimbo la  Chato Dkt. Medard Kalemani mbali nakuipongeza serikali kwa kuendelea kuwapambania wakulima amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuchangamkia fursa ya kilimo cha umwagiliaji.

Sauti ya Mbunge wa Chato Dkt Merdad Kalemani

Mbali na uzinduzi huo wilaya ya Chato imesaini mikataba kati ya wakulima na makampuni ya ununuzi wa tumbaku na Mkataba wa makubaliano ya kilimo mkataba kati ya vyama vya ushirika AMCOS na Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko nchini.