Storm FM

Ahukumiwa kunyongwa kwa kumuua mtoto wake Geita

21 June 2024, 2:01 pm

Anord Shemas aliyepatikana na hatia ya kumuua mtoto wake. Picha na Kale Chongela

Matukio ya ukatili yanaendelea kuacha maswali mengi kutokana na ndugu wa karibu pamoja na wazazi kutajwa kuhusika kwenye baadhi ya matukio hayo dhidi ya watoto wao.

Na: Kale Chongela – Geita

Mahakama kuu kanda ya Geita imemhukumu kunyongwa hadi kufa Anord Shemas baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mtoto wake, Anna Shemas mwenye umri wa mwezi mmoja kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mtoto huyo hakufanana naye.

Kesi hiyo ya jinai namba 53 ya mwaka 2022, Shemasi alikuwa akikabiliwa na kesi ya  mauaji akidaiwa kuua kwa makusudi mtoto wake, Anna Shemas, Oktoba 19, 2021 katika Kijiji cha Kakumbi kilichopo Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita kinyume na kifungu 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16, kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akitoa hukumu hiyo Juni 19. 2024, jaji mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina amesema upande wa mashtaka umethibitisha pasi na shaka kuwa mshtakiwa alimuua Anna Shemas kwa kukusudia kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16.

Akisoma hukumu hiyo kwa dakika 55, jaji Mhina ameeleza kuwa mahakama baada ya kuangalia ushahidi wa pande zote mbili, mambo ya msingi ya kuthibitishwa ni kuwa kweli mtoto alifariki, kifo kilikuwa sio cha kawaida na kama kweli mshtakiwa alihusika.

Jaji Mhina amesema hakuna ushahidi wa macho unaothibitisha mshtakiwa kuhusika lakini ushahidi wa kimazingira wa mshtakiwa unadhihirisha Anna Shemas ni marehemu.

kwa mujibu wa uchunguzi wa daktari unathibitisha kuwa Anna Shemas hakufa kifo cha kawaida kwa kuwa alinyongwa na kusababisha kukosa hewa na mwili uliokutwa kwenye maji haukuwa na maji tumboni, hivyo kuthibitisha kifo chake hakikuwa cha kawaida.