Storm FM

Jamii yakumbushwa kulea watoto katika misingi ya kidini

23 April 2024, 4:21 pm

Askofu wa kanisa la African inland church dayosisi ya Geita Reuben Yusuf Ng’wala. Picha na Joel Maduka

Malezi sahihi ya mtoto hutajwa kuwa kiungo muhimu katika kujenga taifa la kesho, hivyo wazazi na walezi wanahimizwa kuzingatia suala la malezi na makuzi ya mtoto kwenye misingi ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.

Na Joel Maduka – Geita

Jamii imekumbushwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inawalinda watoto dhidi ya vitendo vinavyoweza kuwaathiri kisaikolojia na hata vile ambavyo kuhatarisha maisha yao.

Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la Africa inland church dayosisi ya Geita Reuben Yusufu Ng’wala wakati wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shirika la Compation ambalo lengo lake ni kuwakomboa watoto na vijana kutoka kwenye mazingira ya umasikini.

Askofu Ng’wala amesema ni wajibu wa kanisa pamoja na waumini kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuwalinda watoto dhidi ya vitendo hatarishi na kuwaelekeza katika matendo yampendezayo Mwenyezi Mungu.

Sauti ya Askofu Reuben Ng’wala
Baadhi ya watoto na vijana waliowezeshwa kupitia shirika la Compation ambalo limeadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Picha na Joel Maduka

Akimwakilisha mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Geita, afisa tarafa wa wilaya ya Geita Bw. Alex Araka ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza wazazi kuwafundisha watoto umuhimu wa kumjua Mwenyezi Mungu.

Sauti ya Afisa tarafa Ndg. Alex Araka

Shirika la Compation kupitia huduma ya watoto na vijana  limesaidia vijana wengi wasomi ambapo wengine wameajiriwa na wengine kujiajiri kupitia huduma hiyo. Shirika hilo lilianzishwa mwaka 1999 mkoani Arusha na hadi sasa lina vituo zaidi ya 500 kwenye makanisa mbalimbali kwaajili ya kutoa msaada kwa watoto na vijana.