

11 November 2024, 1:33 pm
Katika kuhakikisha mfumo wa M-MAMA unatoa huduma kwa tija, waandishi wa habari kutoka redio za kijamii kanda ya ziwa wamejengewa uwezo namna unavyofanyakazi ili kuwaambia wananchi.
Na Daniel Magwina:
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba ametoa wito kwa Redio za jamii kusaidia kuelimisha umma juu ya mfumo wa M-MAMA unaotoa fursa ya usafiri wa dharura kwa Mama mjamzito na mtoto mchanga kuanzia kwenye ngazi ya jamii hadi kwenye vituo vya kutolea huduma wakati wa dharura kwa kupiga namba 115 bure.
Akifungua semina ya mafunzo kwa Redio za jamii kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ikiwemo Storm FM kwenye hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza Novemba 08, 2024 Dkt. Lebba amesema wanahabari kutoka kwenye Redio za kijamii wana nafasi kubwa ya kusaidia wananchi kuweza kufahamu mfumo huo ulioletwa mahsusi kwa ajili ya kuokoa maisha.
Huduma hii hutolewa kwa wanawake waliopata changamoto baada ya kujifungua ndani ya siku 42 pamoja na watoto wachanga ambao wana umri siku 0 hadi 28 hawa ndio walenga wa mfumo huu iwapo siku zimezidi utakuwa nje ya mpango huu.
Kwa upande wake Mratibu wa M-mama Mkoa wa Mara Stanley Kajuna Amesema wanufaika wa kuduma hiyo ya dharura ya M-mama ni mama aliyejifungua ndani ya siku 42 na watoto wenye siku 28,huduma ya usafiri wa dharura kwa walengwa inapatikana kwa kupiga simu bure kwenda namba 115.
Kwa upande wao baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria kikao hicho wameelezea walichojifunza na matarajio yao wakirejea katika maeneo yao ya kazi.
Huduma ya M-MAMA ni mfumo wa usafirishaji wa dharura wa wajawazito na watoto wachanga pindi wanapokabiliwa na changamoto za kiafya wawapo mbali na vituo vya kutolea huduma za afya kwa kupiga simu 115 bila malipo na ulizinduliwa Kitaifa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Samia suluhu Hassan April 2022.