Storm FM
Storm FM
30 April 2026, 7:34 pm

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Geita imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisheria kwa kufikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali yanayofanyiwa uchunguzi.
Na: Ester Mabula
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Geita imewafikisha Mahakamani watumishi sita wa mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Geita kwa tuhuma ya ubadhirifu wa shilingi 261,424,788.85 uliofanyika katika akaunti ya Mirathi ya Mahakama kuu Masjala ndogo ya Geita.
Watumishi hao waliwalipa wanufaika nane wasio na madai yoyote ya mirathi mahakamani kwa lengo la kurudisha fedha hizo kwa watumishi na kwa wenza wao kupitia miamala ya kibenki na mitandao ya simu kinyume na utaratibu.
Watumishi hao waliohusika na ubadhirifu huo ni VERONICA JAPHET MWANASENGA ambaye ni Hakimu Mahakama ya Mwanzo Nyankumbu, Bulemo Yuda Mswaga -Afisa Hesabu mkuu, MERCY GEOFFREY MAGEZI-Msaidizi wa kumbukumbu na WILLIAM JOHN MBWAMBO-Dereva kutoka Mahakama ya Hakimu mkazi Geita.

Kwa kushirikiana na watumishi kutoka idara zingine za serikali, Upendo Aloyce Rugohe -Tabibu Halmashauri ya wilaya Wanging’ombe Mkoani Njombe ,Felix Casmiry Swaty Mtumishi wa chuo kikuu kishirikishi cha Elimu Dar es salaam (DUCE), Salimu Issa Lyimo -Mhaidrolojia wizara ya maji Dodoma, Mgema Magembe Julius -Diwani wa kata ya Majengo iliyopo Monduli Arusha pamoja na wafanyabiashara Amani Idd Abdallah Erick Albert Chitumbi, Michael Samson Chanzi na David George Mrope.
Kufuatia matukio hayo na baada ya kupata vibali kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) watuhumiwa tajwa wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashauri matano katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Geita.
